Njia 9 za kutumia Ili kuwashinda wakatishaji tamaa.

Kwa kuchagua kufanya makubwa ili ufanikiwe,
Kwa kuchagua kuendelea kujifunza na kujaribu vitu vipya,
Utazalisha matokeo ya tofauti, matokeo ambayo hayajazoeleka.
Hilo litaleta kwako kundi kubwa la watu ambao watakukosoa na kukukatisha tamaa.
Kundi hilo litaonekana kuwa na nguvu na kuwa sahihi kwa namna watakavyokudhalilisha.
Lazima uwe imara sana katika kukabili kundi hili, la sivyo hutaweza kufika mbali, utakata tamaa na kuishia njiani.

Kwa kugundua ukubwa wa tatizo hili, Robin anatushirikisha njia tisa za kuwashinda wakatishaji tamaa. Kwa kuzijua njia hizi tisa na kuzifanyia kazi, hakuna atakayeweza kukukatisha tamaa. Na hata pale mtu anapokuja kwako kukukatisha tamaa, unanufaika zaidi na ukatishaji wake tamaa kuliko kuumia.
Njia hizo tisa ni kama ifuatavyo;

  1. Wakatishaji tamaa ni walimu wako wazuri.
    Wanakuonyesha ni maeneo gani una madhaifu au wapi hujiamini.
    Pale mtu anapojaribu kukukatisha tamaa na hilo likakuingia, ni kiashiria kwamba kuna kitu hakipo sawa kwa upande wako.
    Hivyo tumia hilo kutambua wapi una udhaifu na uhakikishe unakuwa imara sana ili yeyote asiweze kukutikisa.
    Kama ni kuboresha zaidi kile unachofanya au kujiamini zaidi, fanya kile kinachohitajika ili wakatishaji tamaa wasiwe na nguvu kwako.
  2. Wanaoumiza wana maumivu.
    Watu wenye maumivu huwa wanahakikisha wanawaumiza na wengine pia.
    Watu waliokata tamaa huwa wanahakikisha wanawakatisha na wengine tamaa pia.
    Hivyo unapoona watu wanakukatisha tamaa, jua tatizo kubwa siyo wewe bali ni wao wenyewe.
    Wanajaribu kutoa kile ambacho tayari kipo ndani yao.
    Hivyo badala ya kuumia, hebu waonee huruma. Maisha yao yameshawaadhibu kiasi kwamba furaha pekee kwao ni kuwaumiza wengine kama wao walivyoumia.
  3. Mwanga hukaribisha kumbikumbi.
    Ukiwasha mwanga kwenye eneo lenye giza, utaleta nuru, lakini pia jua utakaribisha kumbukumbi kuja kwenye mwanga huo.
    Huwezi kuzima mwanga kwa sababu ya kumbukumbi wengi ambao wamekuja. Bado hawawezi kuzuia nuru ya mwanga.
    Kadhalika kwenye kile unachofanya, unapozalisha matokeo bora, utawanufaisha wengi, lakini pia kuna wachache watakaokuja kama wasumbufu.
    Usiache kutoa thamani yako kwa sababu ya hao wachache, achana nao.
  4. Watu walio juu huwa hawahangaiki kuwaangusha wengine.
    Ni watu walio chini ndiyo huwa wanatumia muda na nguvu zao kuwavuta wengine warudi chini.
    Watu waliojuu kwanza hawana hata muda wa kuhangaika na nini wengine wanafanya, wametingwa sana na kile wanachofanya.
    Lakini hata wakiwa na muda huo, wanawasaidia wengine kupanda juu kama wao na siyo kuwashusha chini.
    Ukiona mtu anakukatisha tamaa, jua hakuna kikubwa kinachoendelea kwenye maisha yake, hana kinachomweka bize kupambania ndiyo maana anapata muda wa kuhangaika na mambo yako.
    Je kweli unataka uachane na ndoto zako kubwa kwa sababu ya watu ambao hawana ndoto zozote? Hilo siyo sahihi.
  5. Wenye chuki wamezika ndoto zao kubwa.
    Sifa nyingine ya wakosoaji na wakatishaji tamaa ni hii, wangependa sana kufanya makubwa kama wewe, lakini hawawezi, hivyo wanakuchukia kwa sababu wewe umeweza kile ambacho wao wameshindwa.
    Wenye chuki kwenye ndoto zako kubwa unazofanyia kazi ni wale ambao wamezika ndoto zao kubwa.
    Wangetamani sana na wao wawe kama wewe ila hawawezi, kwa sababu walishakatishwa tamaa na kukubali.
    Hivyo kikubwa wanachoweza ni kukatisha wengine tamaa, usiwasikilize.
  6. Kazi yenye nguvu hugusa pande mbili kubwa.
    Pale unapofanya kazi yoyote yenye nguvu, inayoleta mapinduzi makubwa, utagusa pande kuu mbili.
    Upande wa kwanza ni wale watakaokupenda sana kwa sababu umekuwa mkombozi wao kupitia kazi yako.
    Na upande wa pili ni wale watakaokuchukia sana kwa sababu umevuruga mazoea waliyokuwa nayo.
    Ili upendwe na baadhi, lazima pia uchukiwe na baadhi ya watu.
    Kama unataka usichukiwe na mtu yeyote, jua pia hutaweza kupendwa na yeyote.
    Kama hakuna anayekuchukia maana yake hakuna kazi kubwa na ya kimapinduzi unayofanya, unafanya vitu vya kawaida tu na ambavyo vimezoeleka
  7. Kuelewa kazi ya tofauti lazima mtu awe na jicho la tofauti.Watu wengi hupinga vitu vipya siyo kwa sababu havifai, ila kwa sababu hawavielewi.Ndiyo maana kila aina mpya ya ugunduzi huwa inakutana na upinzani mkali mwanzoni. Unakuwa ni ugunduzi wenye manufaa kabisa, ila kwa sababu watu hawaelewi, wanapinga.Inawachukua muda watu mpaka waje kuelewa ndiyo waone manufaa ya kitu.Hivyo unapofanya kitu kipya na kuleta matokeo ya tofauti na ukapingwa sana, jua siyo kwa sababu hakifai, ila kwa sababu watu hawajakielewa.Usiache kufanya kitu bora kwa sababu watu hawajaelewa, wewe endelea kufanya na siku moja watakuja kuelewa.
  8. Kukosolewa ni dalili ya ushawishi.Kama wanavyosema, mti wenye matunda ndiyo unaopigwa mawe.Kukosolewa na kukatishwa tamaa ni dalili kwamba umekuwa na ushawishi mkubwa, unafanya mambo makubwa.Hakuna mtu anayehangaika na mtu asiye na ushawishi mkubwa.Hivyo tumia kipimo cha wakosoaji na wakatishaji tamaa kujua kwamba ushawishi wako umekuwa mkubwa.
  9. Kazi mpya zinatikisa mazoea.Kuna mazoea ambayo yameshajengeka kwenye kila eneo, na hayo ndiyo yanachukuliwa kama ukweli na kiwango ambacho kila mtu anapimwa nacho.Ukifanya kwa mazoea hayo unazalisha matokeo ya kawaida na utapendwa na wale waliozoea hivyo.Ukifanya kwa namna mpya na ya tofauti utazalisha matokeo ya kipekee, lakini pia utatikisa mazoea yaliyopo.Wale waliozoea mazoea hayo hawatakuacha salama, watakupinga na kukukatisha tamaa kwamba unakwenda kinyume na utaratibu.Lakini hupaswi kuwasikiliza, kwa sababu mapinduzi huwa hayaletwi kwa kukumbatia kilichopo.Tumia njia hizi tisa kuhakikisha unasimama imara kabisa kwenye kile ambacho umechagua kufanya na hakuna yeyote anayeweza kukuyumbisha au kukukatisha tamaa.
  10. La mwisho rafiki yangu ni kwamba zama tunazoishi sasa zina wakatishaji tamaa wengi, usipokuwa imara, hutafika kwenye mafanikio unayoyataka.

Naamini upo kama mimi unapenda uendelee mbele zaidi na kuhakikisha unavuka vikwazo zote zinazoletwa na wakatishaji tamaa wengi ambao wanatuzunguka . Inakutegemea ni sauti gani usikilize sauti ya nje ya hao wakatishaji tamaa,au yako wewe mwenyewe unaokumbia ‘endelea mbele.’

Mwandishi wako akupendaye sana.

Maureen Kemei.

kemeimaureen7@kemeimaureen

http://www.uamshobinafsi.com/wp-admin

By Maureen Kemei

Author, psychologist.

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *