Umuhimu wa kujua kusudi la maisha yako.

Rafiki yangu mpendwa,hatua muhimu katika kujitambua kwenye kuelekea katika ubobezi wako ni kujua kusudi la maisha yako.

Wanasema kusudi lakini siyo moja,unaweza kuwa na makusudi mengi na tofauti katika vipindi mbalimbali vya maisha yako.

Kwa kuanzia na kipindi cha maisha yako,jua kusudi lako kwa sasa. Hapo ndipo pa kuanzia ili uweze kupambana kufikia ubobezi na mafanikio makubwa.

Katika kujua kusudi lako,jiulize maswali haya manne muhimu.

1. Kama ungekuwa na uhuru wa kuipangilia siku yako nzima unavyotaka wewe,ni vitu gani ungefanya kwenye siku yako nzima? Swali hili linakuwezesha kujua vitu unavyovipa vipaumbele kikubwa kwenye maisha yako.

2. Ni vitu gani unapenda kufuatilia sana? Kwenye simu yako ni picha gani zipo kwa wingi zaidi? Swali hili linakuwezesha kujua vitu unavyopenda zaidi kufuatilia na kufanya.

3. Ni vitu gani ukifanya unajiskia furaha na mwenye nguvu zaidi? Vitu gani huchoki kuvifanya ? Angalia kwenye mwezi uliopita na orodhesha vyote ulivyofanya kisha jua vipi vilikupa furaha na nguvu zaidi. Swali hili linakuwezesha kujua vitu ambavyo unafanya kutoka ndani ya nafsi yako kweli na siyo unafanya kwa sababu unalazimishwa kufanya.

4. Ni vitu gani ulipendelea sana kufanya ulipokuwa na miaka 12 mpaka 15 ? Na je tangu umekua mapenzi yako kwenye vitu hivyo yameendaje? Swali hili linakuwezesha kujua vitu unavyopenda kufanya kutoka ndani ya nafsi yako na siyo kwa kulazimishwa au kwa sababu unalipwa. Katika umri wa miaka 12 mpaka 15 mtu anakuwa anapambana kuwa huru na hapo hupenda vitu ambavyo ni vya tofauti kabisa na wengine . Katika umri huo mtu anakuwa halisi zaidi kwake. Zaidi ya umri huo jamii inaanzia kumharibu mtu na kumwambia nini anapaswa kufanya na nini hapaswi .

Maswali hayo manne yatakupa mwanga mkubwa wa nini kusudi lako.

Majibu utakayoyapata yanaweza kuwa yanakupa hofu kwa sababu ni vitu ambavyo jamii imekuwa inakukataza usifanye.

Na unapoona kitu kinatoka ndani yako lakini unakuwa na hofu kubwa kukifanya ,basi jua hicho ndiyo sahihi kwako.

Rafiki yangu baada ya kujua kusudi lako kupitia maswali hayo, kuna hatua muhimu za kuchukua.

1. Ipangilie siku yako kwa namna ambayo utafanya zaidi vile unavyovipenda kufanya na siyo tu vile unavyolazimika kufanya.

2. Tafuta jumuiya ya watu wanaofanya kile unachopenda kufanya na jiunge nao, unapofanya na wengine unakuwa na msukumo mkubwa . Pia tafuta menta wa kukufundisha na kukuongoza Ili uweze kufikia ubobezi kwenye eneo hilo.

3. Soma sana kuhusu eneo hilo ulilochagua . Soma historia la eneo hilo kwa undani kabisa. Soma wasifu wa wale waliofanikiwa sana kwenye eneo hilo. Soma maendeleo na vitu vipya vinavyogunduliwa kwenye eneo hilo. Kwa kifupi unapaswa kujua kila kitu kuhusu eneo ulilochagua. Kwa kuwa ni kitu unachopenda na ulichochagua mwenyewe, kujifunza hakutakuwa kugumu kwako.

4. Changanya makusudi uliyonayo pamoja. Kama unapenda kitu zaidi ya kimoja,angalia jinsi unavyoweza kuviunganisha pamoja Ili uzalishe kitu cha kipekee sana. Hii ndiyo Siri kubwa ya wale walioweza kuja na vitu vipya na vya kipekee na kufanikiwa sana. Walileta pamoja vitu vyote walivyopenda kufanya kisha wakazalisha kitu cha tofauti.

5. Chukua hatua. Kila siku chukua hatua katika kufanya yale yaliyo kwenye kusudi lako . Kila siku kuwa bora kwa asilimia 1 zaidi katika ufanyaji. Na kila mara fanya majaribio mbalimbali Ili uweze kuwa bora kwenye kile unachofanya.

Kwa kuchukua hatua hizi tano, utaweza kuanza kuishi kusudi la maisha yako. Lakini bado watu hawatakuacha kirahisi,bado utakutana na vikwazo na changamoto. Hivyo unapaswa kuwa imara sana.

Mwandishi wako akupendaye sana.

Maureen Kemei.

kemeimaureen7@gmail.com

By Maureen Kemei

Author, psychologist.

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *