Kikwazo kikubwa kinachofanya watu kushindwa kuishi maisha halisi kwao ni kutokujitambua na hivyo kujikuta wakiiga watu wengine.
Na hii imekuwa hatari sana kwenye zama hizi ambapo ushauri wa maisha umekuwa mwingi. Wengi wanajikuta wakiiga wengine kwa namna mbalimbali hivyo licha ya kuweka juhudi na muda,bado hawafanikiwi.
Ni muhimu sana kujitambua wewe mwenyewe ili uweze kuishi maisha halisi kwako.
Kwenye ustoa,kuna vitu vinne muhimu ambavyo mtu anapaswa kuvijua kuhusu yeye mwenyewe ili aweze kujitambua na kuishi maisha halisi kwake.
Kitu cha kwanza ni asili yetu kama binadamu. Sisi binadamu tuna asili inayotutofautisha na viumbe wengine wote hapa ulimwenguni.
Na asili yetu kubwa ni uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi. Hicho ni kitu ambacho kinapatikana kwa binadamu pekee na chenye nguvu kubwa.
Lazima ujue asili hii na uweze kuitumia Ili kuishi maisha halisi kwako. Kila mara jiulize kama umefikiri na kufanya maamuzi au unafuata tu mkumbo. Wanyama huwa wanafuata mkumbo,wewe usiwe kama wao.
Kitu cha pili ni uwezo na vipaji ulivyonavyo. Kila mtu ana uwezo wa kipekee na mkubwa sana ambao amezaliwa nao. Uwezo ambao hauwezi kupatikana kwa mtu mwingine yeyote. Na kila mtu ana vipaji vyake,vitu anavyoweza kuvifanya vizuri na kwa upekee mkubwa.
Jua uwezo wako na vipaji vyako na kuvitumia,maana hiyo ndiyo njia pekee ya kuishi maisha halisi kwako. Uzuri ni kwamba uwezo mkubwa na vipaji vyetu huwa havipotei,vinabaki na sisi maisha yetu yote.
Kitu cha tatu bahati tunazokutana nazo kwenye maisha. Kuna mambo mengi yanayotokea kwenye maisha yako, ambayo hayapo ndani ya udhibiti wako. Hayo yote huwa yanakuja na fursa nzuri ambazo ukiweza kuzitumia utaishi maisha halisi kwako.
Bahati zinaweza kuwa eneo ulilozaliwa,elimu uliyopata,watu unayokutana nao na kadhalika. Tangu umezaliwa mpaka sasa umepitia mambo mengi ambayo ukiweza kuyatumia vizuri utaishi maisha halisi.
Kitu cha nne ni utashi wetu ambao unabebwa na kusudi na ndoto tunazokuwa nazo. Yale unavyochagua kufanya kwenye maisha yako,ambayo yanatokana na msukumo ulio ndani yako yanakufanya uishi maisha halisi kuliko yale uliyoiga.
Hivyo ni muhimu sana ujue kusudi lako na uwe na ndoto kubwa zinazotoka ndani yako ili kuwa na maisha halisi kwako.
Ustoa unasisitiza sana tujitambue sisi wenyewe ili tusisumbuke na mambo yasiyo sahihi kwetu. Maana kuna mambo wengine wanaweza kufanya na wakafanikiwa vizuri,ila sisi tukafanya tusifanikiwe.
Kuchukua hatua; kuepuka kupoteza muda na nguvu, tujitambue na kuishi kulingana na upweke na utofauti wetu. Kuiga maisha ya wengine ndiyo chanzo cha wengi kuwa na maisha magumu.
Mwandishi wako.
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com