Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini mtego mkubwa wa ufanisi ni pale mtu unapodhani unapaswa kufanya kila kinachokuja mbele yako, au kila ambacho watu wanataka ufanye.
Pata picha unaweza kuanza na nia nzuri kwamba umalize haraka majukumu madogo madogo yaliyo mbele yako ili upate muda kwa majukumu makubwa.
Lakini unapokuja kushtuka unagundua majukumu madogo madogo yanazidi kuongezeka, huku majukumu makubwa yakiwa yanazidi kuahirishwa.
Hivi ndivyo watu wengi wanavyoyapoteza maisha yao, kwa kujikuta muda umeenda sana lakini hakuna mkubwa waliyofanya.
Wanahangaika na mambo madogo madogo yanayokuja mbele yao, wakiamini watayamaliza, lakini hayaishi.
Chukua mfano wa mwandishi ambaye jukumu lake kuu ni kuandika. Lakini kwanza anaanza kwa kujibu barua pepe ambazo ametumiwa, akiamini anazimaliza ndiyo aanze kuandika.
Wakati anamaliza kujibu barua pepe, zile alizoanza kujibu zinakuwa zinajibiwa tena hivyo inabidi azijibu tena. Kinachotokea ni siku inakuwa imeisha, amechoka lakini jukumu kuu la uandishi halijafanyika.
Kabla hujafanya maamuzi, ni lazima ujue kwamba hata uwe na mbinu bora kiasi gani ya ufanisi, unapochagua kufanya kitu kimoja maana yake umechagua kutokufanya kitu kingine.
Rafiki yangu muda unaotenga kufanya kitu hiki ni muda ambao huwezi kuutumia kufanya kitu kile.
Kuchukua hatua; rafiki yangu bila ya kukubali hili na kupangilia vizuri yale ambayo mtu unafanya, ufanisi utazidi kukupoteza badala ya kukusaidia. Maana utafanya mengi sana, lakini yasiyo na tija.
Hakikisha kila siku unafanya kile chenye tija pekee na kuachana na kile kinachokuchosha na kukupotezea muda wako.
Akupendaye sana,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.